Jun 19, 2013

JOHN MNYINKA ADAI KUWA KESHO WATAWASHA MOTO TENA JIJINI ARUSHA


WAKATI Jeshi la Polisi Mkoani Arusha ikiendelea kumsaka Mwenyekiti wa Chadema Freeman Mbowe na Mbunge wa Jimbo la Arusha Mjini Godbless Lema,Mbunge wa Ubungo John Mnyika kesho atawasha moto mwingine wa maombolezo uliotawanywa kwa mabomu jana.

Mnyika atakuwa msatari wa mbele kuongoza wafuasi wa Chadema kuaga miili ya watu watatu waliouawa katika shambulio la kigaidi Jumamosi iliyopita kwenye Uwanja wa Soweto.


Mbali na Mnyika zoezi hilo pia litasimamiwa na wabunge wanne wa Chadema walioachiwa huru kwa dhamana leo kwakua upelelezi wa kesi zao hazijakamilika.


wabunge hao waliachiwa huru kwa dhamana katika Kituo Kikuu cha Polisi Mkoani hapo kabla ya kufikishwa Mahakamani na kutakiwa kurudi Polisi Julai 22 mwaka huu .


Wabunge hao Said Arfi (Mpanda Mjini), Tundu Lissu (Singida Mashariki), Mustapha Akunaay (Mbulu) na Joyce Mukya (Viti Maalumu), walipewa dhama hiyo majira ya saa nane mchana.


Kabla ya Wabunge hao kuachiwa huru kwa dhamana, maelfu ya wafuasi wa Chama hicho walijazana katika Mahakama hiyo wakisubiri msafara wa wabunge hao, na mara baada ya kupewa taarifa kwamba wabunge hao wameachiwa huru wakiwa Polisi,maandamano makubwa yakaelekea katika Kituo cha Polisi.


Akizungumza baada ya dhamana hiyo Tundu Lissu alisema kwamba, Jeshi la Polisi limempa hasara kubwa baada ya kuvunja mawani yake na kwamba hivi sasa hawezi kufanya kazi yoyote mpaka atakapo pata mawani mapya.



Mbunge wa Ubungo John Mnyika aliyefika jijini Arusha kwa ajili ya kuwawekea dhama wabunge hao alisema kwamba, Chama hicho bado kitaendelea na mipango yake ya kuomboleza na kutoa heshima za mwisho kwa marehemu waliouawa kwa shambulio la bomu katika mkutano wa kisiasa wa Chama hicho Juni 15 mwaka huu katika Uwanja wa Soweto, marehemu hao ni pamoja na Judith Moshi, Ramadhan Juma na Amir Ally, waliofariki kwenye mlipuko wa bomu.


Akizungumza na waandishi wa Habari baada ya kutoka Polisi Mnyika alisema, "Kesho tutaendelea na zoezi la kuwaaga wenzetu waliofariki dunia katika mkutano wetu, na watazikwa kwa heshima zote za Chama,zoezi litaanzia kanisani kabla ya kwenda katika eneo maalum ilipoandaliwa kwa ajili ya kutoa heshima za mwisho".


Hata hivyo Mnyika alikataa kujata jina la kanisa muda wala eneo iliyopangwa kwa madai kwamba ni mapema sana.

                                                              SOURCE: MPEKUZI BLOG

IDD SIMBA NA WENZAKE WAACHIWA HURU KATIKA KESI YA KUHUJUMU UCHUMI


Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam leo hii imemwachiria huru Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika la Usafiri Dar es Salaam (UDA), Idd Simba pamoja na Mkurugenzi wa Bodi hiyo ambaye alikuwa Diwani wa Kata Sinza (CCM), Salum Mwaking’inda vile vile Meneja Mkuu wa shirika hilo Victor Milanzi na Mkurugenzi wa Kampuni ya Simon Group , Simon Kisena waliokuwa wakikabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi wa shirika hilo.

Mahakama imewaachia huru washitakiwa kwa sababu Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), Dk Eliezer Feleshi alliwasilisha hati ya kutokuwa na haja ya kuendelea kuwashitaki washitakiwa hao chini ya kifungu cha 91(1) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai ya mwaka 2002.

Simba anayetetewa na wakili maarufu nchini Alex Mgongolwa walifikishwa na mahakamani hapo kwa mara ya kwanza Mei 27 28 mwaka jana wakikabiliwa na makosa ya kula njama, matumizi mabaya ya madaraka na kughushi na hujumu uchumi.

Hivyo kuanzia sasa, washitakiwa hao wapo huru.

VURUGU ZA ARUSHA: CHADEMA YAGOMA KUTOA USHAHIDI POLISI, LEMA AJIFICHA KWA MCHOMA NYAMA ....WAANDISHI WAAMBULIA KICHAPO


Wabunge wanne wa Chadema, Said Arfi (Mpanda Mjini), Tundu Lissu (Singida Mashariki), Mustapha Akunaay (Mbulu) na Joyce Mukya (Viti Maalumu) wamekamatwa wakituhumiwa kuhusika na mkusanyiko usio halali kwenye Uwanja wa Soweto jana.

Mkuu wa Operesheni wa Polisi, Kamishna Paul Chagonja alisema jana kwamba pamoja na wabunge hao pia wamewakamata watu wapatao 60 kutokana na vurugu zilizozuka jana baada ya Polisi kuwatawanya kwenye uwanja huo waliokuwa wamekusanyika kuomboleza vifo vya watu watatu; Judith Moshi, Ramadhan Juma na Amir Ally waliofariki kwenye mlipuko wa bomu uliotokea kwenye uwanja huohuo, Jumamosi iliyopita.

Mbali ya viongozi hao, alisema wanawasaka Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema.

“Tunawasaka wabunge ili tuwajumuishe na watu hawa kwa kosa la kuhusika na mkusanyiko usiokuwa halali. Hadi sasa tumefanikiwa kulinasa gari la Mbowe,” alisema Chagonja.

Pia kamatakamata hiyo imemkumba Mpigapicha wa Kituo cha Televisheni cha Channel Ten, Ashraf Bakari. Polisi walilazimika kutumia nguvu kuwatawanya waombolezaji hao.

Awali, Kamishna Chagonja alisema jana asubuhi kuwa wamelazimika kuzuia viwanja hivyo kutumika baada ya wamiliki wake, AICC kuzuia shughuli za Chadema kwenye eneo lao na kwamba upelelezi bado unaendelea katika viwanja hivyo.

Kamishna Chagonja aliwaonyesha waandishi wa habari barua aliyosema imeandikwa na uongozi wa AICC kuzua Chadema kuendelea kuutumia Uwanja wa Soweto.

Mabomu yarindima

Dalili za kuzuka kwa vurugu zilianza kuonekana asubuhi baada ya polisi kuzingira uwanja huo na kuzuia watu waliokuwa wameanza kufurika katika eneo hilo kuanzia saa moja kuingia kwa ajili ya maombolezo.

Wakati Polisi wakiwa uwanjani, wananchi walijaa nje ya uwanja na kuonekana kama wamewazingira.

Viongozi wa Chadema wakiongozwa na Mbowe waliwasili uwanja hapo yapata saa nane mchana na kukuta zuio hilo na kuanza kuzungumza na wananchi ingawa FFU walikuwa wakiwataka watu kutawanyika. Mabomu yalianza kurindima wakati Arfi aliposimama na kuwahimiza wananchi kuelekea Hospitali ya Mount Meru kwa ajili ya kuaga miili ya marehemu.

“Tuna muda mfupi sana wa kuzungumza hapa, tunaomba wote tuelekee Hospitali ya Mount Meru kuaga miili ya marehemu kwa sababu uwanja huu umezuiwa na polisi,” alisema Arfi kabla ya kukatishwa na milipuko ya mabomu.

Awali, Lissu ambaye pia ni Mwanasheria wa Chadema alitoa msimamo wa chama hicho kuwa Mwenyekiti wao, Mbowe na Lema hawatatoa ushahidi wa tukio la bomu wala kujisalimisha polisi kwa sababu hawana imani na jeshi hilo.

“Namtaka Chagonja atangulie mahakamani, tutakutana hukohuko. Mbowe na Lema hawatatoa ushahidi wala kujisalimisha polisi...
” alisema Lissu na kuongeza:

“Kisheria haiwezekani polisi ambao ndiyo watuhumiwa ndiyo wadai kukabidhiwa ushahidi ili wauharibu.”

Mapema Kamishna Chagonja aliwataka Mbowe na Lema kutoa ushahidi wa polisi kuhusika na tukio la kurusha bomu kwenye mkutano wa Chadema la sivyo polisi watatumia sheria kuwalazimisha kufanya hivyo.

Hekaheka

Baada ya polisi kuanza kutupa mabomu saa 8.45 mchana, wabunge, viongozi waandamizi wa Chadema na watu waliokuwa wamekusanyika walilazimika kutimua mbio.

Watu walioshuhudia tukio lile wanasema viongozi hao akiwamo Mbowe na mwenzake Lissu walikimbilia kwenye magari yao. Lema alilazimika kukimbilia kwa wachoma nyama ya nguruwe, (kitimoto) kwenye maeneo ya Kaloleni.

Kabla ya polisi kurusha bomu mahali alipokuwapo Lema, mbunge huyo alisikika akisema:

“Jaribuni kuvumilia, tunajaribu kuwasiliana Serikali ya Mkoa, ili watupe kibali cha kuleta miili ya wapendwa wetu hapa, kuweni wastaarabu kwa sababu mbele yetu kuna wana usalama ambao wanalinda amani, ingawa kufa ni kufa tu, wenzetu wameshakufa na sisi ipo siku tutakufa, lakini kila anayetangulia lazima tumzike kwa heshima zote.”

Kauli hiyo iliwachefua polisi ambao walishatangaza amri ya watu kutawanyika katika viwanja hivyo na kwamba hakutakuwa na suala la kuaga miili ya watu hao katika eneo hilo. Ghasia hizo zilisababisha kusimama kwa shughuli za biashara na kijamii kwa muda jijini Arusha huku watu waliokuwa katika nyumba zilizokuwa karibu na maeneo yalikorushwa mabomu wakilazimika kutoka nje kupata hewa safi baada ya nyumba hizo kujaa hewa ya mabomu.

Polisi waliokuwa wakirusha mabomu waliwakimbiza wananchi hadi maeneo ya Sakina huku wakiendelea kufyatua mabomu kila walipoona mkusanyiko wa watu.

Katika eneo la Kaloleni
, mkabala na Ofisi ya Mtendaji wa Kata hiyo baadhi ya wafuasi wa Chadema walichoma matairi barabarani na kusababisha ifungwe. Pia walichoma matairi katika eneo la Mianzini


Katika eneo la Tanki la Maji
, Barabara ya kwenda Moshi, baadhi ya wafuasi wa Chadema walipanga mawe barabarani na kusababisha msongamano wa magari.

Katikati ya jijini Arusha barabara zilikuwa hazipitiki kutokana na nyingine kufungwa na kusababisha usumbufu mkubwa.

Waandishi nao matatani

Katika vurugu hizo, baadhi ya waandishi wa habari walishambuliwa na polisi. Hao ni pamoja na Mwandishi Mwandamizi wa Gazeti la The Citizen, Zephania Ubwani ambaye kabla ya kuchomoka katika mikono ya askari, alikuwa akiwaonyesha kitambulisho chake cha kazi.

Hata hivyo, askari hao walimtishia kumtandika na kisha kumwambia aondoke katika eneo hilo kwa kuwa haijalishi yeye ni nani.

Mwingine ni mwandishi wa gazeti la Nipashe, Cnythia Mwilolezi ambaye alilazimika kuacha viatu na vitendea kazi vyake katika Uwanja wa Soweto na kukimbilia kwenye moja ya nyumba zilizopo jirani na eneo la tukio.

Katibu Msaidizi wa Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Arusha, Moses Kilyinga alipigwa na polisi baada ya kuonekana akichukua maelezo.

Kilyinga ambaye alishambuliwa na askari hao alisema mara baada ya askari hao kumkamata, alijitambulisha lakini hawakumwelewa na wakaendelea kumchapa kabla ya kufanikiwa kuchomoka.

Polisi wavamia hospitali

Wakati baadhi ya majeruhi wakidai kushuhudia polisi wakiwapiga risasi watu waliokuwa wakimkimbiza mtu aliyerusha bomu katika tukio la Jumamosi, askari hao juzi walifika katika Hospitali ya Seliani saa mbili usiku wakitaka kumchukua mmoja wa majeruhi kwa mahojiano kuhusiana na tukio hilo. Hata hivyo, hawakufanikiwa baada ya mgonjwa kutokomea kusikojulikana baada ya kupata taarifa za kutaka kuhusishwa na tukio hilo.

Ingawa si polisi wala Chadema waliokuwa tayari kumtaja mgonjwa huyo, inaelezwa kwamba majeruhi anayesakwa ni Abdallah Alila aliyekaririwa na vyombo vya habari jana na juzi akidai kumshuhudia aliyerusha boma akiondoka kwenye moja ya magari ya polisi.

Hata hivyo, Kamishna Chagonja jana alisema kwamba jeshi lake linapenda kushirikiana na raia kupata taarifa na si kutumia nguvu katika kukusanya ushahidi wake.

LUNDENGA AMTIMUA MREMBO JUKWAANI BAADA YA KUTINGA NA KIVAZI CHA NUSU UCHI....


MWENYEKITI wa Kamati ya Mashindano ya Miss Tanzania, Hashimu Lundenga Jumamosi iliyopita alimtimua mshiriki wa shindano la Redd’s Miss Morogoro 2013, Saphina Chumba (20) jukwaani wakati shindano hilo lilipokuwa likiendelea.
Tukio hilo lilitokea Jumamosi iliyopita katika Ukumbi wa Hoteli ya Kitalii ya Nashera mjini hapa wakati mrembo huyo alipokuwa akiwania kuvaa taji la mkoa huo.
 Kisa cha mrembo huyo aliyevalia namba 5 kutimuliwa ni kukiuka maadili na kanuni za mashindano hayo kwa kuvaa nusu utupu mbele ya mgeni rasmi ambaye alikuwa Mbunge wa Kilosa, Mustapha Mkulo na mbele ya Kamati nzima ya Miss Tanzania.
Baada ya kuona jinsi alivyovaa, Lundenga na kamati yake walikubaliana kumtimua mshiriki huyo kwa kumwita Jaji Mkuu wa shindano, Alex Niktasi na kumtaka amuondoe haraka.
Mbali na Chumba, pia jaji alimtimu mrembo mwingine aliyevalia namba 8, Neema Joel (20) kutokana na kushiriki shindano  hilo mara mbili mwaka huu, inadaiwa mara ya kwanza alishiriki mkoani Arusha.
Lundenga alipohojiwa na mwandishi wetu alisema kamati yake inataka kuendeleza nidhamu tangu ngazi ya chini, hivyo hawawezi kuruhusu utovu wa nidhamu.

KAHABA APEWA KICHAPO KIKALI BAADA YA KUNASWA AKIJUZA JIRANI NA MSIKITI


Kahaba  mmoja   alijikuta akiambulia kichapo kikali toka kwa vijana wa kiislamu baada ya kunaswa akijiuza karibu na msikiti wao.....
 
Tukio hilo lilishuhudiwa na wanahabari wetu majira ya usiku jirani na msikiti huo uliopo nyuma ya Corner Bar, Kijitonyama jijini Dar ambapo mwanamke huyo na wenzake walikamatwa na baadhi ya vijana waumini wa Kiislamu waliokerwa na kitendo cha wao kutoa huduma haramu ya ngono maeneo hayo.


Baada ya wenzake kufanikiwa kutoka nduki mwanamke huyo alishuhudiwa akila bakora kisha akapelekwa katika Kituo cha Polisi Kijitonyama, Dar akaunganishwa na wengine waliokamatwa usiku huo.

Ilielezwa kuwa wanawake hao wamekuwa wakiuza miili kwa wanaume karibu na msikiti huo na pembezoni mwa baa hiyo.

Ilisemekana kuwa kumekuwa na kawaida ya wanawake hao kusimama maeneo ya nyumba hiyo ya ibada na kufanya biashara hiyo huku wakichafua mazingira kwa kutupa ovyo kondomu na kujisaidia maeneo hayo.
 Wakati mwanamke huyo akicharazwa bakora, nguo ya ndani ilimvuka huku akipiga kelele kuwa hatarudia kufanya hivyo na kama akirudia basi akatwe kichwa.

Kutokana na kukerwa na vitendo hivyo, vijana hao wanaofanya ibada katika msikiti huo, waliamua  kuwatafuta vijana wa ulinzi shirikishi na kuwapa kazi hiyo ya kuwakamata na kuwacharaza bakora kisha kuwapeleka katika kituo hicho cha polisi.
 

“Tumeamua kuwakamata na kuwacharaza bakora, hawana ustaarabu wala busara hawa, wanakojoa na kutupa kondomu  hovyo, “ alisikika mmoja wa vijana hao.
 
Mmoja wa vijana hao aliyekuwa akisimamia kwa karibu zoezi hilo, aliwaambia waandishi wetu kuwa wameamua kufanya hivyo na litakuwa zoezi endelevu kutokana na wanawake hao kutokuwa wasikivu kwani kila wanapoambiwa juu ya kukaa mbali na nyumba hiyo ya ibada hawasikii.

Alisema kuwa siku moja wanawake hao walimtoa udhu muumini mmoja ambaye alikuwa akienda kuswali alfajiri baada ya kumshika na kusababisha akose kuhudhuria swala siku hiyo.



Hata hivyo, wakati mahojiano yanaendelea, mmoja wa askari waliokuwa zamu aliamuru mwanamke huyo aingizwe lokapu kusubiri kesho yake aunganishwe na wenzake kisha wapelekwe mahakamani.

Habari zilizotufikia  ni kwamba baada ya kufikishwa mahakamani na kukutwa na kosa la uzururaji, wakahukumiwa kifungo cha miezi sita jela au faini ya shilingi elfu hamsini ambapo walilipa kiasi hicho na bado wanaendelea na biashara hiyo maeneo hayo.

SERIKALI YA MAPINDUZI ZANZIBAR YATOA SALAMU ZA RAMBIRAMBI KWA MKUU WA MKA WA ARUSHA


Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imetuma salamu za rambi mbali kwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mh. Magesa Muhongo kutokana na vifo vya wananchi watatu wa Mkoa huo vilivyotokea kufuatia mripuko wa bomu uliotokea juzi katika viwanja vya Soweto Jijini Arusha.

Watu wasiopungua 70 waliripotiwa kujeruhiwa wakati wa mripuko huo kwenye mkutano wa hadhara wa kampeni za uchaguzi katika Kata ya Soweto wa Chama cha Demokrasia ya Maendeleo { Chadema }.

Katika Taarifa ya rambi rambi ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar iliyotumwa kwa Mkuu huyo wa Mkoa wa Arusha na kutiwa saini na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alielezea kupokea kwa masikitiko na huzuni taarifa ya shambulio la kigaidi la bomu lililotokea tarehe 15 Juni mwaka 2013.

Balozi Seif alisema Taifa kwa mara nyengine tena limekumbwa na msiba wa njama za kigaidi zilizoua na kujeruhi rMkuu wa Koa wa Arusha aia wema wasio na hatia sambamba na tukio jengine linalofanana na hilo lililogharimu roho za wananchi wengine wakati wakiwa katika ibada Kanisani.

Balozi Seif alisema kwa niaba ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Wananchi na yeye binafsi anatuma salamu hizo za rambi rambi kutokana na maafa hayo na kuwaombea marehemu malazi pema na majeruhi wapone haraka ili waungane na wenzao katika ujenzi wa Taifa.


Halkadhalika Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inaiunga mkono Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania katika jitihada zake za kupambana na ugaidi wa aina yoyote hapa Nchini.

Alieleza kwamba SMZ na Wananchi wa Zanzibar wako pamoja na wenzao katika kipindi hiki kigumu cha huzuni na maombolezo na kuwaomba wafiwa wawe na moyo wa ustahamilivu, uvumilivu na subra katika kipindi hichi.

Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania imeamua kutenga shilingi Milioni Mia Moja { 100,000,000/-} kama zawadi kwa kwa mtu ye yote atakayetoa Taarifa zitakazofanikisha kunaswa kwa mhalifu au watu wenye mtandao wa ulipuaji wa mabomu hapa Nchini.

Jun 18, 2013

KESI YA MENEJA WA MALAWI CARGO ANAYETUHUMIWA KUOMBA RUSHWA YA NGONO KWA MFANYAKAZI WAKE YAANZA KUUNGURUMA MAHAKAMANI


ALIYEKUWA  Meneja wa Kampuni ya Malawi Cargo tawi la Mbeya Evason Mwale(49) raia wa nchi jirani ya Malawi, amefikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Mbeya akituhumiwa kujihusisha na Rushwa ya Ngono.

Mwendesha mashtaka wa Serikali Basilius Namkambe akisoma Mashtaka ya mtuhumiwa huyo mbele ya Hakimu mkazi wa mahakama hiyo Gilbert Ndeuluo alisema Mtuhumiwa anashtakiwa kwa makosa mawili ambayo ni Rushwa ya Ngono kinyume cha kifungu cha 25 cha Sheria ya kuzuia na kupambana na Rushwa namba 11 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2007.

Namkambe alidai mahakamani hapo kuwa mtuhumiwa anashtakiwa kwa kosa lingine la matumizi mabaya ya madaraka kinyume cha kifungu cha 31 cha Sheria ya kuzuia na kupambana na Rushwa namba 11 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2007.
  
Alisema mtuhumiwa huyo alitenda kosa hilo April 11, Mwaka huu katika Hoteli moja iliyopo Iyunga Jijini Mbeya ambapo alikamatwa akitaka kujihusisha na rushwa ya Ngono na Mke wa Mfanyakazi wake.

Kwa upande wake Hakimu Mkazi Ndeoruo aliahirisha kesi hiyo hadi Julai 1, Mwaka huu kwa ajili ya kuanza kusikiliza ambapo pia alisema Dhamana  iko wazi kwa Mtuhumiwa kuwa na wadhamini wawili wenye hati za mali isiyohamishika yenye thamani ya Shilingi Milioni 10, Barua zinazotambuliwa na mamlaka, ambapo pia mtuhumiwa  anatakiwa kuacha hati zake za kusafiria na kutoruhusiwa kutoka nje ya Jiji la Mbeya bila ruhusa ya mahakama.

Awali  ilidaiwa kuwa Meneja huyo alitaka kujihusisha na Rushwa na Mke wa Mfanyakazi wake wa nyumbani ambaye alimfukuza kazi na baadaye alimtumia Mkewe ili amrudishe kazini baada ya kufanya naye mapenzi.

BAADA YA NAPE KUITUHUMU CHADEMA, MBOWE NAYE AFUNGUKA NA KUDAI KUWA BOMU LILIRUSHWA NA FFU NA USHAHIDI ANAO


MWENYEKITI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe amefichua siri kuhusu tukio la mlipuko wa bomu lililotokea jusi katika viwanja vya Soweto, jijini Arusha.

Katika kauli yake jana, Mbowe ameibua tuhuma nzito dhidi ya Jeshi la Polisi, ambapo alidai kuwa askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) ndiye aliyerusha bomu hilo.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa,baada ya kutembelea majeruhi katika Hospitali ya Selian, Mbowe alisema chama chake kina ushahidi wa kutosha juu ya askari huyo kurusha bomu.

Mbowe ambaye pia ni kiongozi wa kambi ya upinzani bungeni,alisema wamefanikiwa kupata ushahidi wa kutosha juu ya tukio hilo baya linalochafua taswira ya nchi.

Alisema chama chake kipo tayari kuweka ushahidi huo hadharani, iwapo Serikali itaendelea kufanya siasa na kuficha ukweli.


“Tunao ushahidi wa kutosha, ikiwamo wa picha za video unaoonyesha shambulio la bomu na risasi lilivyofanyika katika mkutano wangu jusi eneo la Soweto.

“Picha zinaonesha wazi aina ya silaha zilizotumika kwenye shambulio lile ni tatu, bomu la gurumeti ambalo lilitupwa na askari wa FFU aliyekuwa kwenye uniform.

“Kutokana na ushahidi huu tulikuwa tumewaeleza Polisi kama wataendelea kuficha tutaueleza umma na tutaiambia dunia, kwani aina ya silaha zilizotumika ni SMG na bastola.

“Makasha ya risasi kama ushahidi wa jambo hili zilizotumika tuliyaokota eneo la tukio na tayari tumeyarekodi na kuyakabidhi kwa askari waliokuwa wakichunguza tukio lile,” alisema Mbowe.

Hata hivyo Mbowe alipinga tamko la Serikali kupitia Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Uratibu na Bunge), William Lukuvi na kusema kauli yake ni ya kitoto mbele ya jamii.

“Kauli ya Serikali kupitia kwa Lukuvi kwamba vurugu zilisababishwa na vikundi, wanasiasa na mashirika yasiyo ya kiserikali ambavyo havijulikani ni sawa na kuwadhihaki Watanzania,” alisema.

Kutokana na hali hiyo Mbowe alisema tayari wanasheria wa chama hicho akiwemo Mabere Marando, Tundu Lissu na Profesa Abdallah Safari wanashughulikia suala hilo.

Alisema baada ya polisi huyo kurusha bomu, alikimbilia katika gari ya Toyota Land Cruizer yenye rangi ya bluu akiongozana na askari mwenzake ambapo gari hilo liliondoka kwa kasi, huku likisindikizwa kwa kukingwa na gari ya TDI hadi kituo cha polisi.

CATHY WA BONGO MOVIE ALIA NA USHIRIKINA ULIPO NDANI YA TASNIA HIYO....AWATAKA WASANII WAMRUDIE MUNGU

Mwigizaji wa Bongo, Sabrina Rupia ‘Cathy’  naye amenyanyua kinywa chake na kuonesha jinsi gani anakerwa na wasanii wanaoshinda kwa waganga ili kutafuta ustaa.

Akiongea na mwandishi  wetu hivi karibuni, Cathy alisema kuna baadhi ya wasanii (hakuwataja majina) wamekuwa na tabia za kuzunguka kwa waganga wakitafuta kuwa juu katika tasnia ya filamu suala ambalo halipendezi na kuwasihi wawe na hofu ya Mungu.
“Vifo vya wasanii vimetokea vingi sana, nilidhani kutokana na vifo hivyo wangepata hofu ya Mungu na kuacha mambo yasiyofaa vikiwemo vitendo vya kishirikina lakini hawakomi, wananikera sana. Ipo siku wataumbuka kwani Mungu siyo binadamu,” alisema Cathy.

MSHIRIKI WA KIUME TANZANIA ( NANDO ) YUKO HATARINI KUONDOLEWA BIG BROTHER....KURA YAKO INAHITAJIKA KUMUOKOA

Ni wiki tatu zimepita tukishuhudia Eviction shows tatu zilizowapa tiketi za kurudi makwao washiriki 6 mpaka sasa, na tumeshuhudia mshiriki wetu Feza Kessy akiponea kwenye tundu la sindano baada ya kura za wa Tanzania na wa Afrika kumuokoa, sasa ni zamu ya Nando ambaye yuko hatarini wiki hii.

Big Brother jana ametaja majina ya washiriki 7 ambao wako hatarini kutoka wiki hii na kati yao yupo kijana mpole, mtanashati, ‘handsome’ Nando anaeiwakilisha Tanzania, ikiwa ndio mara yake ya kwanza kupendekezwa .
Washiriki wengine walipigiwa kura nyingi kutoka wiki hii ni love birds Bolt na Betty, ambao hii si mara yao ya kwanza kupendekezwa baada ya kuponea chupuchupu kwa mara kadhaa.
Kenya wiki hii iko salama kwa mshiriki wao mmoja aliyesalia Annabel, japo kuwa alipendekezwa kutoka wiki hii lakini kilichomuokoa ni yeye kuwa mkuu wa nyumba ya Diamond, hivyo amepata favor ya kujiokoa mwenyewe na nafasi yake akampendekeza Motamma wa Botswana.

Kwa ujumla walioingia wiki hii ni Nando wa Tanzania, Natasha wa Malawi, Oneal wa Botswana, Motamma wa Botswana, Betty wa Ethiopia, Bolt wa Sierra Leon na Elikem wa Ghana.
Tanzania bado ina nafasi nzuri sababu washiriki wote wawili Nando na Feza wapo mjengoni na ndio maana unakila sababu ya kumpigia kura mara nyingi uwezavyo Nando ili aweze kubaki wiki hii. 

Washiriki wawili kati ya saba waliopendekezwa watapita kwenye mlango wa ‘EXIT’ mjengoni hapo Jumapili hii (June 23) wakati wa Eviction Show.

Tumpigie  kura  mtanzania  Nando....

Twitter Delicious Facebook Digg Stumbleupon Favorites More

 
Design by Free WordPress Themes | Bloggerized by Lasantha - Premium Blogger Themes | Enterprise Project Management